Zaburi - Sura ya 33

Zaburi - Sura ya 33

1Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

2Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

3Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.

4Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.

5Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.

6Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.

7Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala.

8Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche.

9Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.

10Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu.

11Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.

12Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

13Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia.

14Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani.

15yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote.

16Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu.

17Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.

18Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.

19Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.

20Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.

21Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.

22Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.