Zaburi - Sura ya 35

Zaburi - Sura ya 35

1Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.

2Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.

3Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako.

4Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya.

5Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.

6Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia.

7Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.

8Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.

9Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.

10Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.

11Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua.

12Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa.

13Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu.

14Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye.

15Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi.

16Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno.

17Bwana, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba.

18Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.

19Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e.

20Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila.

21Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona.

22Wewe, Bwana, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami.

23Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu.

24Unihukumu kwa haki yako, Ee Bwana, Mungu wangu, Wala wasinisimangize.

25Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza.

26Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu.

27Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake.

28Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.