Zaburi - Sura ya 36
1Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.
2Kwa maana hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa.
3Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema.
4Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii.
5Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni, Uaminifu wako hata mawinguni.
6Haki yako ni kama milima ya Mungu, Hukumu zako ni vilindi vikuu, Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.
7Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhili zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.
8Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako, Nawe utawanywesha mto wa furaha zako.
9Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru.
10Uwadumishie wakujuao fadhili zako, Na wanyofu wa moyo uaminifu wako.
11Mguu wa kiburi usinikaribie, Wala mkono wa wasio haki usinifukuze.
12Huko ndiko walikoanguka wafanyao maovu; Wameangushwa chini wasiweze kusimama.