Zaburi - Sura ya 37

Zaburi - Sura ya 37

1Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili.

2Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka.

3Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.

4Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.

5Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.

6Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri.

7Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila.

8Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.

9Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi.

10Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.

11Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani.

12Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake.

13Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.

14Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu.

15Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika.

16Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi.

17Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali Bwana huwategemeza wenye haki.

18Bwana anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele.

19Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba.

20Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao Bwana watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka.

21Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.

22Maana waliobarikiwa na yeye watairithi nchi, Nao waliolaaniwa na yeye wataharibiwa.

23Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake.

24Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza.

25Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.

26Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa.

27Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele.

28Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.

29Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele.

30Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu.

31Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi.

32Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha.

33Bwana hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa.

34Wewe umngoje Bwana, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona.

35Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni.

36Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana.

37Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.

38Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa.

39Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.

40Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.