Zaburi - Sura ya 38

Zaburi - Sura ya 38

1Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako.

2Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata.

3Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu.

4Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno.

5Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu.

6Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika.

7Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu.

8Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu.

9Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako, Kuugua kwangu hakukusitirika kwako.

10Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.

11Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali.

12Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa.

13Lakini kama kiziwi sisikii, Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake.

14Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, Ambaye hamna hoja kinywani mwake.

15Kwa kuwa nakungoja Wewe, Bwana, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu.

16Maana nalisema, Wasije wakanifurahia; Mguu wangu ukiteleza wajitukuza juu yangu.

17Kwa maana mimi ni karibu na kusita, Na maumivu yangu yako mbele yangu daima.

18Kwa maana nitaungama uovu wangu, Na kusikitika kwa dhambi zangu.

19Lakini adui zangu ni wazima wenye nguvu, Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi.

20Naam, wakilipa mabaya kwa mema, Huwa adui zangu kwa kuwa nalifuata lililo jema.

21Wewe, Bwana, usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami.

22Ufanye haraka kunisaidia, Ee Bwana, wokovu wangu.