Zaburi - Sura ya 4

1Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu.
2Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo?
3Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.
4Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia.
5Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini Bwana.
6Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema? Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
7Umenitia furaha moyoni mwangu, Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai.
8Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.