Zaburi - Sura ya 40

1Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.
2Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.
3Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana
4Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.
5Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki.
6Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
7Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)
8Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
9Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.
10Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa.
11Nawe, Bwana, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.
12Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha.
13Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.
14Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.
15Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!
16Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana.
17Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.