Zaburi - Sura ya 41

1Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu.
2Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake.
3Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.
4Nami nalisema, Bwana, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi.
5Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea?
6Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena.
7Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.
8Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena.
9Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.
10Lakini Wewe, Bwana, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa.
11Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hasimangi kwa kunishinda.
12Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele.
13Na atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.