Zaburi - Sura ya 44

1Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.
2Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao.
3Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia.
4Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.
5Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.
6Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa.
7Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha.
8Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.
9Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu.
10Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka.
11Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa.
12Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao.
13Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
14Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.
15Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika,
16Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.
17Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako.
18Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako.
19Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.
20Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;
21Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo.
22Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa.
23Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa.
24Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?
25Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi.
26Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.