Zaburi - Sura ya 45

Zaburi - Sura ya 45

1Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi.

2Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.

3Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako.

4Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha.

5Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme.

6Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

7Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako.

8Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.

9Binti za wafalme wamo Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki. Mkono wako wa kuume amesimama malkia Amevaa dhahabu ya Ofiri.

10Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.

11Naye mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.

12Na binti Tiro analeta kipawa chake, Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako.

13Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu, Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.

14Atapelekwa kwa mfalme Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri. Wanawali wenzake wanaomfuata, Watapelekwa kwako.

15Watapelekwa kwa furaha na shangwe, Na kuingia katika nyumba ya mfalme.

16Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako, Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.

17Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu Katika vizazi vyote. Kwa hiyo mataifa watakushukuru Milele na milele.