Zaburi - Sura ya 46

1Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
2Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
3Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.
4Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
5Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
6Mataifa yalighadhibika, falme zikataharuki; Alitoa sauti yake, nchi ikayeyuka.
7Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
8Njoni myatazame matendo ya Bwana, Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
9Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari.
10Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu, Nitakuzwa katika mataifa, nitakuzwa katika nchi.
11Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.