Zaburi - Sura ya 47

Zaburi - Sura ya 47

1Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe.

2Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya, Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.

3Atawatiisha watu wa nchi chini yetu, Na mataifa chini ya miguu yetu.

4Atatuchagulia urithi wetu, Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda.

5Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu.

6Mwimbieni Mungu, naam, imbeni; Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni.

7Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili.

8Mungu awamiliki mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu.

9Wakuu wa watu wamekusanyika, Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu. Maana ngao za dunia zina Mungu, Ametukuka sana.