Zaburi - Sura ya 5

Zaburi - Sura ya 5

1Ee Bwana, uyasikilize maneno yangu, Ukuangalie kutafakari kwangu.

2Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.

3Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.

4Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako;

5Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao ubatili.

6Utawaharibu wasemao uongo; Bwana humzira mwuaji na mwenye hila

7Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu.

8Bwana, uniongoze kwa haki yako, Kwa sababu yao wanaoniotea. Uisawazishe njia yako mbele ya uso wangu,

9Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Mtima wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza.

10Wewe, Mungu, uwapatilize, Na waanguke kwa mashauri yao. Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, Kwa maana wamekuasi Wewe.

11Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia.

12Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; Bwana, utamzungushia radhi kama ngao.