Zaburi - Sura ya 50

Zaburi - Sura ya 50

1Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake.

2Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika.

3Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote.

4Ataziita mbingu zilizo juu, Na nchi pia awahukumu watu wake.

5Nikusanyieni wacha Mungu wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.

6Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.

7Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena, Mimi nitakushuhudia, Israeli; Mimi ndimi niliye MUNGU, Mungu wako.

8Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako, Na kafara zako ziko mbele zangu daima.

9Sitatwaa ng'ombe katika nyumba yako, Wala beberu katika mazizi yako.

10Maana kila hayawani ni wangu, Na makundi juu ya milima elfu.

11Nawajua ndege wote wa milima, Na wanyama wote wa mashamba ni wangu

12Kama ningekuwa na njaa singekuambia, Maana ulimwengu ni wangu, navyo viujazavyo.

13Je! Nile nyama ya mafahali! Au ninywe damu ya mbuzi!

14Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.

15Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.

16Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?

17Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

18Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.

19Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.

20Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.

21Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.

22Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.

23Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.