Zaburi - Sura ya 51

Zaburi - Sura ya 51

1Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu.

2Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.

3Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.

4Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.

5Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.

6Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,

7Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji

8Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi.

9Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.

10Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu

11Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

12Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.

13Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako.

14Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako.

15Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako.

16Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.

17Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

18Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu.

19Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako.