Zaburi - Sura ya 55

Zaburi - Sura ya 55

1Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.

2Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua.

3Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi.

4Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia.

5Hofu na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza.

6Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe.

7Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani.

8Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.

9Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.

10Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo ndani yake;

11Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.

12Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione.

13Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.

14Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.

15Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.

16Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa;

17Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.

18Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu, Maana walioshindana nami walikuwa wengi.

19Mungu atasikia na kuwajibu; Ndiye Yeye akaaye tangu milele. Mageuzi ya mambo hayawapati hao, Kwa hiyo hawamchi Mungu.

20Amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye, Amelihalifu agano lake.

21Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi.

22Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.

23Nawe, Ee Mungu, utawatelemsha, Walifikilie shimo la uharibifu; Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao, Bali mimi nitakutumaini Wewe.