Zaburi - Sura ya 56

1Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita.
2Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi.
3Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe;
4Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?
5Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya.
6Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.
7Je! Wataokoka kwa uovu wao? Ee Mungu, uwaangamize kwa hasira yako.
8Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)
9Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;
10Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake.
11Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
12Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu; Nitakutolea dhabihu za kushukuru.
13Maana umeniponya nafsi yangu na mauti; Je! Hukuizuia miguu yangu isianguke? Ili nienende mbele za Mungu Katika nuru ya walio hai.