Zaburi - Sura ya 57

Zaburi - Sura ya 57

1Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.

2Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.

3Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake

4Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.

5Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.

6Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake!

7Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi,

8Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.

9Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.

10Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni.

11Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.