Zaburi - Sura ya 58

Zaburi - Sura ya 58

1Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki? Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?

2Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu; Katika nchi mnapima udhalimu wa mikono yenu.

3Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.

4Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.

5Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.

6Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee Bwana, uyavunje magego ya wana-simba.

7Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.

8Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,

9Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto.

10Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.

11Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko Mungu Anayehukumu katika dunia.