Zaburi - Sura ya 60

Zaburi - Sura ya 60

1Ee Mungu, umetutupa na kututawanya, Umekuwa na hasira, uturudishe tena.

2Umeitetemesha nchi na kuipasua, Upaponye palipobomoka, maana inatikisika.

3Umewaonyesha watu wako mazito, Na kutunywesha mvinyo ya kutuyumbisha.

4Umewapa wakuogopao bendera, Ili itwekwe kwa ajili ya kweli.

5Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono wako wa kuume, utuitikie.

6Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi.

7Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,

8Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.

9Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hata Edomu?

10Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu?

11Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai.

12Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.