Zaburi - Sura ya 61

Zaburi - Sura ya 61

1Ee Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu.

2Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda.

3Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.

4Nitakaa katika hema yako milele, Nitaikimbilia sitara ya mbawa zako

5Maana Wewe, Mungu, umezisikia nadhiri zangu. Umewapa urithi wao waliogopao jina lako.

6Utaziongeza siku za mfalme, Miaka yake itakuwa kama vizazi vingi.

7Atakaa mbele za Mungu milele, Ziagize fadhili na kweli zimhifadhi.

8Ndivyo nitakavyoliimbia jina lako daima, Ili niondoe nadhiri zangu kila siku.