Zaburi - Sura ya 65

Zaburi - Sura ya 65

1Ee Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.

2Wewe usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.

3Ingawa maovu mengi yanamshinda, Wewe utayafunika maasi yetu.

4Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako.

5Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana,

6Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi.

7Wautuliza uvumi wa bahari, Uvumi wa mawimbi yake, Na ghasia ya mataifa;

8Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.

9Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.

10Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake.

11Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.

12Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vyajifunga furaha.

13Na malisho yamevikwa kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, naam, yanaimba.