Zaburi - Sura ya 69

Zaburi - Sura ya 69

1Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu.

2Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha.

3Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu wangu.

4Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.

5Ee Mungu, unajua upumbavu wangu, Wala hukufichwa dhambi yangu.

6Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe, Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi. Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe, Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.

7Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.

8Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.

9Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.

10Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.

11Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.

12Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.

13Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.

14Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.

15Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze, Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.

16Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.

17Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi.

18Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie.

19Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote.

20Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.

21Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.

22Meza yao mbele yao na iwe mtego; Naam, wakiwa salama na iwe tanzi.

23Macho yao yatiwe giza wasione, Na viuno vyao uvitetemeshe daima.

24Uimwage ghadhabu yako juu yao, Na ukali wa hasira yako uwapate.

25Matuo yao na yawe ukiwa, Pasiwe na mtu wa kukaa hemani mwao.

26Maana wanamwudhi mtu uliyempiga Wewe, Wanasimulia maumivu ya hao uliowatia jeraha.

27Uwaongezee uovu juu ya uovu, Wala wasiingie katika haki yako.

28Na wafutwe katika chuo cha uhai, Wala pamoja na wenye haki wasiandikwe.

29Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Mungu, wokovu wako utaniinua.

30Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani.

31Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng'ombe, Au ndama mwenye pembe na kwato.

32Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.

33Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake.

34Mbingu na nchi zimsifu, Bahari na vyote viendavyo ndani yake.

35Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda, Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.

36Wazao wa watumishi wake watairithi, Nao walipendao jina lake watakaa humo.