Zaburi - Sura ya 7

1Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
2Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.
3Bwana, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya, Ikiwa mna uovu mikononi mwangu,
4Ikiwa nimemlipa mabaya Yeye aliyekaa kwangu salama; (Hasha! Nimemponya yeye Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;)
5Basi adui na anifuatie, Na kuikamata nafsi yangu; Naam, aukanyage uzima wangu, Na kuulaza utukufu wangu mavumbini.
6Bwana uondoke kwa hasira yako; Ujiinue juu ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu.
7Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale.
8Bwana atawaamua mataifa, Bwana, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao.
9Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki.
10Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo.
11Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.
12Mtu asiporejea ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari;
13Naye amemtengenezea silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto.
14Tazama, huyu ana utungu wa uovu, Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo.
15Amechimba shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya!
16Madhara yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini.
17Nitamshukuru Bwana kwa kadiri ya haki yake; Nitaliimbia jina la Bwana aliye juu.