Zaburi - Sura ya 71

Zaburi - Sura ya 71

1Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele.

2Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe.

3Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.

4Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu,

5Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu.

6Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima.

7Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.

8Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa.

9Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.

10Kwa maana adui zangu wananiamba, Nao wanaoniotea roho yangu hushauriana.

11Wakisema, Mungu amemwacha, Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya.

12Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.

13Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.

14Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote.

15Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.

16Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.

17Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.

18Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako.

19Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

20Wewe, uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya, Utatuhuisha tena. Utatupandisha juu tena Tokea pande za chini ya nchi.

21Laiti ungeniongezea ukuu! Urejee tena na kunifariji moyo.

22Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu. Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli.

23Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, Na nafsi yangu uliyoikomboa.

24Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.