Zaburi - Sura ya 73

Zaburi - Sura ya 73

1Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao.

2Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza.

3Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki.

4Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu.

5Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu.

6Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo.

7Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.

8Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.

9Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani.

10Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao.

11Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?

12Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi.

13Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa.

14Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi.

15Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako.

16Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu;

17Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao.

18Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika.

19Namna gani wamekuwa ukiwa mara! Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho.

20Ee Bwana, kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao.

21Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma,

22Nalikuwa kama mjinga, sijui neno; Nalikuwa kama mnyama tu mbele zako.

23Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika mkono wa kuume.

24Utaniongoza kwa shauri lako, Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu.

25Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe.

26Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele.

27Maana wajitengao nawe watapotea; Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe.

28Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU, Niyahubiri matendo yako yote.