Zaburi - Sura ya 74

1Ee Mungu, mbona umetutupa milele? Kwa nini hasira yako inatoka moshi Juu ya kondoo wa malisho yako?
2Ulikumbuke kusanyiko lako, Ulilolinunua zamani. Ulilolikomboa liwe kabila ya urithi wako, Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.
3Upainulie miguu yako palipoharibika milele; Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.
4Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako; Wameweka bendera zao ziwe alama.
5Wanaonekana kama watu wainuao mashoka, Waikate miti ya msituni.
6Na sasa nakishi yake yote pia Wanaivunja-vunja kwa mashoka na nyundo.
7Wamepatia moto patakatifu pako; Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.
8Walisema mioyoni mwao, Na tuwaangamize kabisa; Mahali penye mikutano ya Mungu Wamepachoma moto katika nchi pia.
9Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii, Wala kwetu hakuna ajuaye, hata lini?
10Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini? Adui alidharau jina lako hata milele?
11Mbona unaurudisha mkono wako, Naam, mkono wako wa kuume, Uutoe kifuani mwako, Ukawaangamize kabisa.
12Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani, Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi.
13Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako, Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji.
14Wewe uliviseta vichwa vya lewiathani, Awe chakula cha watu wa jangwani.
15Wewe ulitokeza chemchemi na kijito; Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote.
16Mchana ni wako, usiku nao ni wako, Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.
17Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia, Kaskazi na kusi Wewe ulizitengeneza.
18Ee Bwana, uyakumbuke hayo, adui amelaumu, Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako.
19Usimpe mnyama mkali nafsi ya hua wako; Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
20Ulitafakari agano; Maana mahali penye giza katika nchi Pamejaa makao ya ukatili.
21Aliyeonewa asirejee ametiwa haya, Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.
22Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.
23Usiisahau sauti ya watesi wako, Ghasia yao wanaokuondokea inapaa daima.