Zaburi - Sura ya 75

Zaburi - Sura ya 75

1Ee Mungu, twakushukuru. Twakushukuru kwa kuwa Jina lako li karibu; Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu.

2Nitakapoufikia wakati ulioamriwa, Mimi nitahukumu hukumu za haki.

3Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki, Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake.

4Naliwaambia waliojivuna, Msijivune; Na wasio haki, Msiiinue pembe.

5Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi.

6Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima.

7Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu.

8Maana mkononi mwa Bwana mna kikombe, Na mvinyo yake inatoka povu; Kumejaa machanganyiko; Naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia Watazifyonza na kuzinywa.

9Bali mimi nitatangaza matendo yako milele, Nitamwimbia Mungu wa Yakobo.

10Pembe zote za wasio haki nitazikata, Na pembe za mwenye haki zitainuka.