Zaburi - Sura ya 76

1Katika Yuda Mungu amejulikana, Katika Israeli jina lake ni kuu.
2Kibanda chake pia kiko Salemu, Na maskani yake iko Sayuni.
3Huko ndiko alikoivunja mishale ya uta, Ngao, na upanga, na zana za vita.
4Wewe U mwenye fahari na adhama, Toka milima ya mateka.
5Wametekwa wenye moyo thabiti; Wamelala usingizi; Wala hawakuiona mikono yao Watu wote walio hodari.
6Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, Gari na farasi wameshikwa na usingizi mzito.
7Wewe ndiwe utishaye, naam, Wewe; Naye ni nani awezaye kusimama ufanyapo hasira?
8Toka mbinguni ulitangaza hukumu; Nchi iliogopa, ikakaa kimya.
9Mungu aliposimama ili kuhukumu Na kuwaokoa wapole wa dunia wote pia.
10Maana hasira ya binadamu itakusifu, Masalio ya hasira utajifunga kama mshipi.
11Wekeni nadhiri, mkaziondoe Kwa Bwana, Mungu wenu. Wote wanaomzunguka wamletee hedaya, Yeye astahiliye kuogopwa.
12Yeye huzikata roho za wakuu; Na kuwatisha wafalme wa dunia.