Zaburi - Sura ya 77

1Nimpazie Mungu sauti yangu, Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia.
2Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika.
3Nilipotaka kumkumbuka Mungu nalifadhaika; Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.
4Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike; Naliona mashaka nisiweze kunena.
5Nalifikiri habari za siku za kale, Miaka ya zamani zilizopita.
6Nakumbuka wimbo wangu usiku, Nawaza moyoni mwangu, Roho yangu ikatafuta.
7Je! Bwana atatupa milele na milele? Hatatenda fadhili tena kabisa?
8Rehema zake zimekoma hata milele? Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote?
9Mungu amesahau fadhili zake? Amezuia kwa hasira rehema zake?
10Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo; Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kuume wake Aliye juu.
11Nitayakumbuka matendo ya Bwana; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.
12Pia nitaitafakari kazi yako yote; Nitaziwaza habari za matendo yako.
13Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu?
14Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.
15Kwa mkono wako umewakomboa watu wako, Wana wa Yakobo na Yusufu.
16Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka,
17Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa.
18Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika;
19Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana.
20Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni.