Zaburi - Sura ya 78

Zaburi - Sura ya 78

1Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.

2Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale.

3Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia.

4Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za Bwana, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya.

5Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao,

6Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao

7Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake.

8Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.

9Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita.

10Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake;

11Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha.

12Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani.

13Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu.

14Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto.

15Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi.

16Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito.

17Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu.

18Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.

19Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani?

20Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama?

21Hivyo Bwana aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli.

22Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake.

23Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni;

24Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni.

25Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.

26Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake.

27Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari.

28Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao.

29Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani;

30Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao

31Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli.

32Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.

33Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha.

34Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.

35Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao.

36Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.

37Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.

38Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote.

39Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi.

40Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani!

41Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.

42Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi.

43Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani.

44Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa.

45Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu.

46Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao.

47Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.

48Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme.

49Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya.

50Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;

51Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.

52Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani.

53Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao.

54Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume.

55Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.

56Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake.

57Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa.

58Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao.

59Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa.

60Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;

61Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi.

62Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake.

63Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,

64Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza.

65Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;

66Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele.

67Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu.

68Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda.

69Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele.

70Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo.

71Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake.

72Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.