Zaburi - Sura ya 79

Zaburi - Sura ya 79

1Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako, Wamelinajisi hekalu lako takatifu. Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.

2Wameziacha maiti za watumishi wako Ziwe chakula cha ndege wa angani. Na miili ya watauwa wako Iwe chakula cha wanyama wa nchi.

3Wamemwaga damu yao kama maji Pande zote za Yerusalemu, Wala hapakuwa na mzishi.

4Tumekuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

5Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele? Wivu wako utawaka kama moto?

6Ukali wako uwamwagie mataifa wasiokujua, Na falme za hao wasioliitia jina lako.

7Kwa maana wamemla Yakobo, Na matuo yake wameyaharibu.

8Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu, Rehema zako zije kutulaki hima, Kwa maana tumedhilika sana.

9Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie, Kwa ajili ya utukufu wa jina lako. Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako.

10Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Kisasi cha damu ya watumishi wako iliyomwagika Kijulike kati ya mataifa machoni petu.

11Kuugua kwake aliyefungwa Na kuingie mbele zako. Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako Uwahifadhi wana wa mauti.

12Uwalipe jirani zetu mara saba vifuani mwao Laumu zao walizokulaumu, Ee Bwana.

13Na sisi tulio watu wako, Na kondoo za malisho yako, Tutakushukuru milele; Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.