Zaburi - Sura ya 80

Zaburi - Sura ya 80

1Wewe uchungaye Israeli, usikie, Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.

2Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase, Uziamshe nguvu zako, Uje, utuokoe.

3Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

4Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?

5Umewalisha mkate wa machozi, Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.

6Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.

7Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

8Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.

9Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.

10Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.

11Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.

12Kwa nini umezibomoa kuta zake, Wakauchuma wote wapitao njiani?

13Nguruwe wa msituni wanauharibu, Na hayawani wa kondeni wanautafuna.

14Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.

15Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.

16Umechomwa moto; umekatwa; Kwa lawama ya uso wako wanapotea.

17Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume; Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako;

18Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma; Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.

19Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.