Zaburi - Sura ya 81

1Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo.
2Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.
3Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu.
4Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.
5Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
6Nimelitenga bega lake na mzigo, Mikono yake ikaachana na kikapu.
7Katika shida uliniita nikakuokoa; Nalikuitikia katika sitara ya radi; Nalikujaribu penye maji ya Meriba.
8Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya, Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza;
9Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine.
10Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.
11Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka.
12Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao.
13Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
14Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;
15Wamchukiao Bwana wangenyenyekea mbele zake, Bali wakati wao ungedumu milele.
16Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.