Zaburi - Sura ya 83

Zaburi - Sura ya 83

1Ee Mungu, usistarehe, Ee Mungu, usinyamae, wala usitulie.

2Maana adui zako wanafanya ghasia, Nao wakuchukiao wameviinua vichwa vyao.

3Juu ya watu wako wanafanya hila, Na kushauriana juu yao uliowaficha.

4Wamesema, Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa, Na jina la Israeli halitakumbukwa tena.

5Maana wanashauriana kwa moyo mmoja, Juu yako wanafanyana agano.

6Hema za Edomu, na Waishmaeli, Na Moabu, na Wahagari,

7Gebali, na Amoni, na Amaleki, Na Filisti, nao wanaokaa Tiro,

8Ashuri naye amepatana nao, Wamewasaidia wana wa Lutu.

9Uwatende kama Midiani, kama Sisera, Kama Yabini, penye kijito Kishoni.

10Ambao waliangamizwa Endori; Wakawa samadi juu ya nchi.

11Uwafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, Na masheki yao wote kama Zeba na Zalmuna.

12Ambao Walisema, Na tutamalaki makao ya Mungu.

13Ee Mungu, uwafanye kama mavumbi ya kisulisuli, Mithili ya makapi mbele ya upepo,

14Kama moto uteketezao msitu, Kama miali ya moto iiwashayo milima,

15Ndivyo utakavyowafuatia kwa tufani yako, Na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.

16Uwajaze nyuso zao fedheha; Wakalitafute jina lako, Bwana.

17Waaibike, wafadhaike milele, Naam, watahayarike na kupotea.

18Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.