Zaburi - Sura ya 85

Zaburi - Sura ya 85

1Bwana, umeiridhia nchi yako, Umewarejeza mateka wa Yakobo.

2Umeusamehe uovu wa watu wako, Umezisitiri hatia zao zote.

3Umeiondoa ghadhabu yako yote, Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.

4Mungu wa wokovu wetu, uturudishe, Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.

5Je! Utatufanyia hasira hata milele? Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi?

6Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha, Watu wako wakufurahie?

7Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

8Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena.

9Hakika wokovu wake u karibu na wamchao, Utukufu ukae katika nchi yetu.

10Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimehusiana.

11Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni.

12Naam, Bwana atatoa kilicho chema, Na nchi yetu itatoa mazao yake.

13Haki itakwenda mbele zake, Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.