Zaburi - Sura ya 86

1Ee Bwana, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji
2Unihifadhi nafsi yangu, Maana mimi ni mcha Mungu. Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
3Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
4Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
5Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.
6Ee Bwana, uyasikie maombi yangu; Uisikilize sauti ya dua zangu.
7Siku ya mateso yangu nitakuita, Kwa maana utaniitikia.
8Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana, Wala matendo mfano wa matendo yako.
9Mataifa yote uliowafanya watakuja; Watakusujudia Wewe, Bwana, Watalitukuza jina lako;
10Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, Wewe ndiwe mfanya miujiza, Ndiwe Mungu peke yako.
11Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;
12Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele.
13Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.
14Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao.
15Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.
16Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako.
17Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.