Zaburi - Sura ya 88

1Ee Bwana, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako.
2Maombi yangu yafike mbele zako, Uutegee ukelele wangu sikio lako.
3Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu.
4Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada.
5Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.
6Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini.
7Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote.
8Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka.
9Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso Bwana, nimekuita kila siku; Nimekunyoshea Wewe mikono yangu.
10Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi?
11Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu?
12Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?
13Lakini mimi nimekulilia Wewe, Bwana, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia.
14Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako?
15Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika.
16Hasira zako kali zimepita juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza.
17Yamenizunguka kama maji mchana kutwa, Yamenisonga yote pamoja.
18Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo gizani.