Zaburi - Sura ya 9

1Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
2Nitafurahi na kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.
3Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako.
4Kwa maana umenifanyia hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki.
5Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele;
6Adui wamekoma na kuachwa ukiwa milele. Nayo miji yao uliing'oa; Hata kumbukumbu lao limepotea.
7Bali Bwana atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
8Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili.
9Bwana atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida.
10Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, Bwana hukuwaacha wakutafutao.
11Mwimbieni Bwana akaaye Sayuni, Yatangazeni kati ya watu matendo yake.
12Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge.
13Wewe, Bwana, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti,
14Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako.
15Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.
16Bwana amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake.
17Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.
18Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.
19Bwana, usimame, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako.
20Bwana, uwawekee kitisho, Mataifa na wajijue kuwa ni binadamu.