Zaburi - Sura ya 90

Zaburi - Sura ya 90

1Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi.

2Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.

3Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu.

4Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.

5Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo.

6Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.

7Maana tumetoweshwa kwa hasira yako, Na kwa ghadhabu yako tumefadhaishwa.

8Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Siri zetu katika mwanga wa uso wako.

9Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite.

10Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.

11Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako?

12Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.

13Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.

14Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.

15Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya.

16Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao.

17Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.