Zaburi - Sura ya 91

1Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
2Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.
3Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.
4Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.
5Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana,
6Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,
7Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe.
8Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.
9Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.
10Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.
11Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.
12Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
13Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
14Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.
15Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;
16Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.