Zaburi - Sura ya 92

Zaburi - Sura ya 92

1Ni neno jema kumshukuru Bwana, Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.

2Kuzitangaza rehema zako asubuhi, Na uaminifu wako wakati wa usiku.

3Kwa chombo chenye nyuzi kumi, Na kwa kinanda, Na kwa mlio wa kinubi.

4Kwa kuwa umenifurahisha, Bwana, Kwa kazi yako; nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.

5Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.

6Mtu mjinga hayatambui hayo, Wala mpumbavu hayafahamu.

7Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;

8Bali Wewe, Bwana, U Mtukufu hata milele.

9Maana hao adui zako, Ee Bwana, Hao adui zako watapotea, Na watendao maovu watatawanyika wote pia.

10Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati, Nimepakwa mafuta mabichi.

11Na jicho langu limewatazama walioniotea, Sikio langu limesikia habari za waovu walionishambulia.

12Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.

13Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.

14Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.

15Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.