Zaburi - Sura ya 94

Zaburi - Sura ya 94

1Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze,

2Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao.

3Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?

4Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi?

5Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako;

6Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima.

7Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.

8Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?

9Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?

10Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue?

11Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.

12Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako;

13Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.

14Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake,

15Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.

16Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu?

17Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya.

18Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.

19Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu.

20Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria?

21Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia.

22Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia.

23Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza.