Zaburi - Sura ya 95

Zaburi - Sura ya 95

1Njoni, tumwimbie Bwana, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.

2Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi.

3Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.

4Mkononi mwake zimo bonde za dunia, Hata vilele vya milima ni vyake.

5Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, Na mikono yake iliumba nchi kavu.

6Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.

7Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!

8Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Meriba Kama siku ya Masa jangwani.

9Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu.

10Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile, Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo, Hawakuzijua njia zangu.

11Nikaapa kwa hasira yangu Wasiingie rahani mwangu.