Zaburi - Sura ya 96

Zaburi - Sura ya 96

1Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Mwimbieni Bwana, nchi yote.

2Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.

3Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake.

4Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.

5Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.

6Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.

7Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu.

8Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake.

9Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.

10Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki; Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike, Atawahukumu watu kwa adili.

11Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, Bahari na ivume na vyote viijazavyo,

12Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;

13Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake.