Zaburi - Sura ya 97

Zaburi - Sura ya 97

1Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, Visiwa vingi na vifurahi.

2Mawingu na giza vyamzunguka, Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.

3Moto hutangulia mbele zake, Nao huwateketeza watesi wake pande zote.

4Umeme wake uliuangaza ulimwengu, Nchi ikaona ikatetemeka.

5Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana, Mbele za Bwana wa dunia yote.

6Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake.

7Na waaibishwe wote waabuduo sanamu, Wajivunao kwa vitu visivyofaa; Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.

8Sayuni imesikia na kufurahi, Binti za Yuda walishangilia, Kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana.

9Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote; Umetukuka sana juu ya miungu yote.

10Enyi mmpendao Bwana, uchukieni uovu; Huwalinda nafsi zao watauwa wake, Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.

11Nuru imemzukia mwenye haki, Na furaha wanyofu wa moyo.

12Enyi wenye haki, mmfurahieni Bwana, Na kulishukuru jina lake takatifu.