Zaburi - Sura ya 98

Zaburi - Sura ya 98

1Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

2Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.

3Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

4Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.

5Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi.

6Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.

7Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.

8Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha.

9Mbele za Bwana; Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili.