Zaburi - Sura ya 99

1Bwana ametamalaki, mataifa wanatetemeka; Ameketi juu ya makerubi, nchi inatikisika.
2Bwana katika Sayuni ni mkuu, Naye ametukuka juu ya mataifa yote.
3Na walishukuru jina lake kuu la kuhofiwa; Ndiye mtakatifu.
4Nguvu za mfalme nazo zapenda hukumu; Wewe ndiwe uliyeithibitisha adili; Ulifanya hukumu na haki katika Yakobo.
5Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni penye kiti cha miguu yake; Ndiye mtakatifu.
6Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia;
7Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao. Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa.
8Ee Bwana, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu; Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe Ingawa uliwapatiliza matendo yao.
9Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.