Ufunuo wa Yohana - Sura ya 18

Ufunuo wa Yohana - Sura ya 18

1Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake.

2Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza;

3kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.

4Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.

5Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.

6Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu.

7Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.

8Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.

9Na hao wafalme wa nchi, waliozini naye na kufanya anasa pamoja naye, watalia na kumwombolezea; wauonapo moshi wa kuungua kwake;

10wakisimama mbali kwa hofu ya maumivu yake, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu, Babeli, mji ule ulio na nguvu! Kwa kuwa katika saa moja hukumu yako imekuja.

11Nao wafanya biashara wa nchi walia na kumwombolezea, kwa sababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena;

12bidhaa ya dhahabu, na fedha, na kito chenye thamani, na lulu, na kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na hariri, na nguo nyekundu; na kila mti wa uudi, na kila chombo cha pembe, na kila chombo cha mti wa thamani nyingi, na cha shaba, na cha chuma, na cha marimari;

13na mdalasini, na iliki, na uvumba, na marhamu, na ubani, na mvinyo, na mafuta ya mzeituni, na unga mzuri, na ngano, na ng'ombe, na kondoo, na farasi, na magari, na miili na roho za wanadamu.

14Na matunda yaliyotamaniwa na roho yako yamekuondokea; na vitu vyote vilivyo laini na vitu vya fahari vimekupotea; wala watu hawataviona tena kamwe.

15Na wafanya biashara ya vitu hivyo, waliopata mali kwake, watasimama mbali, kwa hofu ya maumivu yake; wakilia na kuomboleza,

16wakisema, Ole, ole, mji ule mkuu! Uliovikwa kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na nguo nyekundu, na kupambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu;

17kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa. Na kila nahodha na kila aendaye mahali popote kwa matanga, na mabaharia, nao wote watendao kazi baharini, wakasimama mbali;

18wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio mfano wa mji huu mkubwa!

19Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa.

20Furahini juu yake, enyi mbingu, nanyi watakatifu na mitume na manabii; kwa maana Mungu amehukumu hukumu yenu juu yake.

21Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa.

22Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yo yote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa;

23wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako.

24Na ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.