Ufunuo wa Yohana - Sura ya 21

1Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.
2Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
4Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.
5Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.
6Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.
7Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
8Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.
9Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.
10Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu;
11wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri;
12ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli.
13Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu.
14Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
15Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake.
16Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa.
17Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika.
18Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi.
19Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi;
20wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto.
21Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.
22Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake.
23Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
24Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.
25Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku.
26Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake.
27Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.